You are on page 1of 2

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

TAARIFA KWA UMMA


UFAFANUZI KUHUSU MADAI YA WASIOKOPA KUDAIWA MIKOPO
1.0

UTANGULIZI
Kumekuwepo na taarifa zilizotolewa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo
vya habari, hasa gazeti la Jamboleo toleo namba 2541 la 23 Agosti, 2016
kuhusu Bodi ya Mikopo kuwadai wasionufaika na mikopo. Taarifa hizi
zinalenga kuleta hofu na mkanganyiko usiokuwa wa lazima kwa wadau.
Kufuatia hatua hiyo Bodi ya Mikopo inapenda kutoa ufafanuzi wa suala hili
kama ifuatavyo:-

2.0

MADAI KUHUSU KUDAIWA MIKOPO KWA WALE WASIONUFAIKA


Bodi ya Mikopo inapenda kuufahamisha Umma kuwa database yake ya
wanufaika wa mikopo ina taarifa zote muhimu zilizo sahihi. Hii inatokana na
utunzaji mzuri wa kumbukumbu za ukopeshaji kuanzia hatua ya utoaji
mikopo (loan allocation and disbursement) hadi urejeshaji wake (loan
repayment). Kutokana hamasa na elimu inayotolewa, kumekuwepo na
mwitikio mkubwa wa wanufaika wa mikopo na waajiri wao kujitokeza na
kuanza kurejesha mikopo. Hivyo, katika utekelezaji wa jukumu hilo,
tumebaini kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadaiwa kwamba
ama hawakuwahi kukopa au hawajawahi kufikia kiwango cha elimu ya juu.
Hadi sasa, imebainika kuwepo kwa baadhi ya wanufaika ambao wanadai
hawakujua iwapo fedha walizopatiwa na serikali wakati huo zilikuwa za
mkopo. Pia kuna wachache ambao vyeti vyao vilitumiwa na ndugu zao kwa
ajili ya masomo ya elimu ya juu. Katika hali hii, mdaiwa atalazimika kumtaja
mtu halisi anayepaswa kukatwa deni hilo ili Bodi iweze kusitisha makato
hayo kwake.
Ili kupata ufumbuzi wa malalamiko hayo, Bodi inawataka walalamikaji
kuzingatia yafuatayo:

2.1 Kwa mtu anayedai kwamba hajasoma elimu ya juu kwa ufadhili
wa serikali au Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu;
mtu huyu awasilishe vielelezo vinavyodhihirisha kuwa hakusomeshwa
kwa ufadhili wa serikali.
2.2 Kwa mtu anayedai amekatwa mshahara ingawa hajawahi
kufikia kiwango cha elimu ya juu; mtu huyo anapaswa kuwasilisha
vielelezo vya kiwango cha elimu yake.
2.3 Iwapo kuna mnufaika wa mkopo anadai amekatwa zaidi ya
kiwango cha mkopo anaodaiwa; mnufaika huyo anapaswa
kuwasilisha vielelezo vinavyothibitisha kumaliza kurejesha deni lake.
Itakapothibitika kuwa kuna makato zaidi yalifanyika, basi kiasi
kilichozidi kitarejeshwa kwa mhusika.
3.0

HITIMISHO
Bodi inapenda kuwahakikishia wadau wake kuwa imetunza vizuri taarifa zote
muhimu za wanufaika wa mikopo ambazo ndizo zinazotumika kwenye zoezi
la urejeshaji wa mikopo. Kasoro ndogo ndogo zinazojitokeza zinatatuliwa
kwa kufanya rejea kwenye kumbukumbu zilizopo.
Aidha, Bodi inaendelea kuwahimiza wanufaika wote wa mikopo ambao
hawajaanza kurejesha mikopo yao kuhakikisha wanawasilisha taaifa zao ofisi
za Bodi au wanajaza taarifa zao kweye fomu Loan Inquiry Form iliyopo
kwenye tovuti ya Bodi na kuituma kwa anuani ya barua pepe
info@heslb.go.tz ili kila mmoja ajulishwe deni lake na kuanza kurejesha.
Kwa mnufaika anayetaka kuanza kurejesha mkopo wake baada ya kuwa
amepata taarifa ya deni lake; aweke fedha kwenye akaunti za Benki
zifuatazo na kisha kuwasilisha hati ya malipo:
A/C No. 2011100205 NMB
A/C No. 01J1028467503 CRDB
A/C No. CCA0240000032 TPB
Imetolewa na:
KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Agosti 24, 2016

You might also like