BUNJU: Mchoma nyama ala kichapo kutoka kwa Meneja,
ODM Asprin ahusishwa na mchepuko..!
Episode I
Siku ya jana nilipata mwaliko warafiki yangu wa hapa JF ambaye pia ni mkuu wa itifaki wa ile mikutaniko yetu yapale Leo Tupo Hapa Pub. Alinialika tukutane katika kijiwe kimoja pale Bunju B kiitwacho Cheers Bar.
Kwa kuwa miye siyo mwenyeji katika maeneo hayo nilijikuta nikiwa ndani ya Bar moja iitwayo Kibila, ikanilazimu niwaulize wahudumu wa pale wakanielekeza mahali ilipo hiyo Bar ya Cheers. Lakini kwa kuwa njaa ilianza kuniuma ikanilazimu kukaa japo nipate supu kwanza wakati nikiendelea kumtafuta mwenyeji wangu ambaye simu yake ilikuwa haipatikani wakati huo. Nilijipa moyo kwa kujiaminisha tu kwamba labda simu yake iliisha chaji.
Naam wakati nikiwa nasubiri supu yangu ya mbavu za mbuzi, mara akaja mdada mmoja maji ya kunde mrefu kidogo na mzuri kwa sura na umbo maana alikuwa amejazia vyema maeneo yake ya makalioni na kifua chake kilikuwa na matiti yaliyotuna vizuri yakiwa sambamba na upana wa kifua chake. Duh nikajikuta namkodolea macho kuanzia juu hadi chini nikijitahidi kusafisha kiwi changu cha macho na kuusifu uumbaji wa maulana.
Wakati nikiwa nimezama kwenye lindi la ndoto fulani tamu nikijihisi najivinjari na yule kimwana mashaallah, nilishtushwa na sauti yake mororo, ambayo ilipenya sawia katika masikio yangu. Ulikuwa ni mtego mwingine kutoka kwa huyo kimwana ulionivunja vunja kabisa nikajikuta nikiishiwa na nguvu kutokana na kukabiliwa na homa ya mahaba.
Samahani kaka, sijui nawezakukaa hapa nikisibiri chipsi zangu aliniomba yule binti huku akiniangalia kwa macho yake malegevu. Miye hoi!
Ndiyo unaweza kukaa bibiye..nilimjibu kwa sauti ya kitetemeshi maana nilipoteza hata kujiamini kwangu.
Naomba niwaambie wanawake wa humu JF. Mkiwaona wanaume zenu hawachepuki basi mjue ni majasiri kweli kweli nawanastahili shahada ya uzamili kwa kufaulu mitihani iliyopo huku duniani. Jamani wanawake wanatutega huko mitaani nyie acheni tu, tena kwa makusudi kabisa. Kama huyu aliyeniomba akae kwenye meza niliyokaa mie wakati zipo meza kedekede zikiwa tupu. Eti sababu ya kutaka kukaa kwenye meza niliyokaa ni ili akae karibu na jikoni akisubiri chipsi zake. Muongo mkubwa, alikuwa anajilengesha tu.
Basi mie nikajisema moyoni,
Hatahili litapita tu, ya nini kumkurubia ibilisi wakati ndiyo kwanza tumetoka kwenye mfungo wa mwezi mtukufu.
Wakati nikijifanya niko bize na simu yangu.. Hamadi, ukaingia ujumbe wa simu ya mkononi kutoka kwa mwana JF mwenzangu Madame B.
Nimekuona hapo baba Ngina Looooooh!!!
Ulisema ujumbe huo. Miye moyo Paaaa, kwa mshituko.., yu wapi huyu mwanamke atakeyenizulia niko na mchepuko wakati nimevamiwa tu! Nilijiuliza huku nikiangaza macho huku na kule kumtafuta alipo.
Ile kuangaza macho huku na kule,nikakutanisha macho yangu na Madame B akiwa amesimama jikoni akinicheka kwa kijino pembe kama vile ananishushua Mwanamke mbaya huyu, najua tu atanizulia kule JF kwamba amenifumania na mchepuko. Nilijisemea moyoni.
Nikiwa bado tumetumbuliana macho. Akaja dada mmoja ambaye nadhani ni dada yake maana wamefanana, wakaondoka nakuingia kwenye gari aina ya Toyota Noah kisha haooo wakaondoka zao, bila hatakunisemesha. Somo likawa limetimia kwamba nilikuwa nimekaa na mchepuko kwa sababu sikupata nafasi ya kujieleza wala kujitetea.
Niliuma midomo kwa hasira nikataka nihame meza, lakini wakati naangaza macho kutafuta meza iliyo tupu,yule binti akanyanyuka kwa madaha bila hata kuniaga na kwenda jikoni kuchukua chipsi zake na yeye akaingia kwenye gari aina ya Toyota Harrier na kuondoka akiniachia msala kwa Madame B.
Naomba Madame B, uje usome utetezi wangu kabla ya kunihukumu tafadhali.